Thursday, September 1, 2011

KIND HEART AFRIKA KWA MALEZI BORA YA MTOTO

SERIKALI imeahidi kukidumisha na kukiendeleza kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Kind Heart Africa.
Hayo yalisemwa mjini Dar es Salaam juzi na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la kituo hicho.
Silaa alikiri kuwa serikali imekuwa ikijitolea katika kuendeleza sekta ya elimu, afya na nyinginezo lakini katika suala la kuwajengea watoto walio katika mazingira magumu maeneo ya kuishi ni kama vile imelitelekeza.
“Kutokana na umuhimu wa kuwathamini na kuhakikisha watoto walio katika mazingira magumu wanaishi salama na kupata huduma muhimu, wakati umefika kwa serikali kuwa mstari wa mbele kuwajengea vituo na kuvidumisha vile vilivyopo,” Meya Slaa alisema.
“Hivyo nitajitahidi pamoja na viongozi wengine waliopo chini yangu kuhakikisha tunakiendeleza kituo hiki, kwa kuwa wanaoishi hapa si wageni bali watoto wetu wa Kitanzania,” alisema.
Aidha aliutaka uongozi wa kituo hicho kuangalia namna itakavyopata wadau wengine watakaoshirikiana nao katika kumalizia baadhi ya maeneo ya kituo hicho.
Jengo lililogharimu sh. milioni 80 lilijengwa kwa udhamini wa raia wa India, Joshi Sathyavan.
Slaa pia alimpongeza Rais na Mchungaji wa madhehebu ya Buddha, Ilukpitiye Pannasekara, ambaye ni raia wa Sri Lanka kwa moyo wa huruma na upendo uliomfanya aje na wazo la kujenga kituo hicho kitakachowasaidia watoto wengi.
“Ni wajibu wa kila mmoja kutoa msaada wowote ukiwamo wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hiki ikiwamo kujenga uzio na majengo mengine ili kitimize malengo yake kwa watoto wetu,” aliongeza.
Naye Mchungaji wa Buddha Pannasekera aliishukuru serikali pamoja na wadhamini mbalimbali waliojitokeza kukamilisha ndoto yake ya kujenga kituo hicho cha kusaidia watoto walio katika mazingira magumu.
Hata hivyo, Mchungaji huyo alitoa wito kwa wadhamini wengine wenye moyo kujitokeza kwa wingi kukiendeleza kituo hicho ambacho kwa sasa kina watoto 27, wakiwemo wasichana watatu na wavulana 24.

No comments:

Post a Comment